Proverbs 29


1 aMtu anayeendelea kuwa na shingo ngumu baada ya maonyo mengi,
ataangamia ghafula, wala hapati dawa.


2 bWenye haki wanapostawi, watu hufurahi;
waovu watawalapo, watu hulia kwa huzuni.


3 cMtu apendaye hekima huleta furaha kwa baba yake,
bali aambatanaye na makahaba hutapanya mali yake.


4 dKwa haki mfalme huipa nchi uthabiti,
bali mfalme aliye na tamaa ya rushwa huiangamiza.


5 eYeyote amsifuye jirani yake isivyostahili,
anautandaza wavu kuitega miguu yake.


6 fMtu mbaya hutegwa na dhambi yake mwenyewe
bali mwenye haki huweza kuimba na kufurahi.


7 gMwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini,
bali mwovu hajishughulishi na hilo.


8 hWenye mzaha huuchochea mji,
bali watu wenye hekima hugeuzia mbali hasira.


9 iKama mwenye hekima akienda mahakamani na mpumbavu,
mpumbavu hukasirika na kudhihaki, wala hakuna amani.


10 jWatu wamwagao damu humchukia mtu mwadilifu
na hutafuta kumuua mtu mnyofu.


11 kMpumbavu huonyesha hasira yake yote,
bali mwenye hekima hujizuia.


12 lKama mtawala akisikiliza uongo,
maafisa wake wote huwa waovu.


13 mMtu maskini na mtu anayeonea wanafanana kwa jambo hili:
Bwana hutia nuru macho yao wote wawili.


14 nKama mfalme akiwaamua maskini kwa haki,
kiti chake cha enzi kitakuwa thabiti siku zote.


15 oFimbo ya maonyo hutia hekima,
bali mtoto aliyeachiwa bila maonyo
humwaibisha mama yake.


16 pWakati waovu wanapostawi,
pia dhambi vivyo hivyo,
lakini wenye haki wataliona anguko lao.


17 qMrudi mwanao, naye atakupa amani,
atakufurahisha nafsi yako.


18 rMahali pasipo na ufunuo, watu kujizuia,
bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.


19 Mtumishi hawezi kuonywa kwa maneno matupu,
ajapoelewa, hataitikia.


20 sJe, unamwona mtu azungumzaye kwa haraka?
Kuna matumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko yeye.


21 Kama mtu akimdekeza mtumishi wake tangu ujanani,
atamletea sikitiko mwishoni.


22 tMtu mwenye hasira huchochea ugomvi,
naye mtu mwenye hasira ya haraka
hutenda dhambi nyingi.


23 uKiburi cha mtu humshusha,
bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu
hupata heshima.


24 vAnayekubaliana na mwizi ni adui wa nafsi yake mwenyewe;
huapishwa lakini hathubutu kushuhudia.


25 wKuwaogopa watu huwa ni mtego,
bali yeyote amtumainiaye Bwana atakuwa salama.


26 xWengi hutafuta kusikilizwa na mtawala,
bali mtu hupata haki kutoka kwa Bwana.


27 yMwenye haki huwachukia sana wasio waaminifu;
waovu huwachukia sana wenye haki.
Copyright information for SwhKC